Ingawa kuna maandiko kadhaa katika lugha ya Kimashami, kamusi hii ni ya kwanza kuandaliwa kwa lugha hii. Kamusi yenyewe imekusudiwa kukidhi mahitaji ya wasomaji wa aina mbili. Kwanza, kama ilivyokusudiwa katika mpangilio wa Mradi wa Lugha za Tanzania, itakidhi mahitaji ya watafiti wa isimu wanapofanya uchunguzi kwa kulinganisha data za lugha mbalimbali. Pili, katika jitihada za kukuza na kuhifadhi lugha za Tanzania, kamusi hii itakidhi mahitaji ya msomaji wa kawaida, hasa yule ambaye lugha yake ya kwanza au lugha ya kwanza ya wazazi wake ni Kimashami. Inatazamiwa kwamba kamusi hii itaweka msingi wa kutengeneza kamusi sanifu ya Kimashami, na kuimarisha vigezo vya tahijia na maandishi kwa jumla katika lugha hii.
